Na Mahmoud Mohamed, Mogadishu
Agosti 31, 2012
Mwandishi wa habari wa Mogadishu Abdifatah Ahmed amepokea vitisho ya
kifo mara kadhaa kutoka kwa wanamgambo katika miaka mitatu iliyopita.
"Hata kama tunakuwa walengwa wa watu wenye msimamo mkali, hatutatishika na vitisho kama hivyo vya uwoga," aliiambia Sabahi.
Ahmed alisema amechukua hatua kadhaa za tahadhari tangu alipoanza kupokea vitisho.
"Baadhi ya hatua nilizochukua ni pamoja na kubadilisha kila mara njia
yangu wakati ninaposafiri baina ya nyumbani na pahali pa kazi, pamoja
na kubadilisha ratiba zangu za kila siku," alisema. Mara nyengine huamua
kusafiri na walinzi."
Kwa waandishi wa habari nchini Somalia, 2012 imekuwa mwaka wa damu.
"Katika muda wa miezi minane ya kwanza ya mwaka huu, waandishi wa
habari 9 wameuwawa na 20 wengine kujeruhiwa katika mikono ya watu wenye
silaha, na kuufanya mwaka huu kuwa mbaya na wa damu zaidi kwa waandishi
wa habari wa Somalia," alisema Abdullahi Mohamed Hassan, mkurugenzi wa
Nyumba ya Vyombo vya Habari Mogadishu, ambayo inashughulikia kukuza
amani na kulinda haki za waandishi wa habari.
Hivi karibuni zaidi, tarehe 12 Agosti, waandishi wa habari wa Somalia Yusuf Ali Osman na Mohamud Beneyste waliuliwa katika mikono ya watu wasiojulikana wenye silaha mjini Mogadishu.
Mohamed Ahmed, mwandishi wa habari mkongwe anayeishi Mogadishu na
kufanya kazi kama mhariri wa tovuti ya habari nchini Somalia, alisema
yeye pia amekuwa akitumiwa ujumbe za vitisho.
"Tangu mwaka 2009, nimepokea barua kadhaa na simu kutoka kwa watu
nisiowajua wanaodai ni kutoka kikundi chenye msimamo mkali cha
al-Shabaab na kutishia kuniua," aliiambia Sabahi. "Wanaweza kuniambia
eti mimi ni adui wa Uislamu na kwamba, Mungu akipenda, mujahidina
watanisaka na kunimaliza."
Ahmed alisema anaogopa kwa sababu wenzake wengi, ambao pia walikuwa wametishiwa, waliuwawa na watu wasiojulikana wenye silaha.
Hata hivyo, Ahmed alisema, "Sijawahi kufikiria kuiacha kazi yangu na
kuikimbia nchi yangu. Kama ningekuwa wa kuacha kazi yangu kwa sababu ya
vitisho vya kipuuzi kama hivyo, hii ingemaanisha kuwa wanamgambo
wamefanikiwa malengo yao na kuvinyamazisha vyombo vya habari."
Abdiaziz Biilo, mwandishi wa habari wa Mogadishu wa Press TV, alisema
kufanya kazi kama mwandishi wa habari nchini Somalia ni changamoto
kubwa sana.
"Kila asubuhi, unaondoka nyumbani kwako na kwenda kazini bila ya
kujua kama utarejea salama au la. Ni mazingira magumu sana na usalama
hauhakikishwi kwa wale wanaofanyakazi katika vyombo vya habari,"
aliambia Sabahi.
"Nimehudhuria mazishi ya waandishi wa habari wenzangu kadhaa ambao
walipigwa bunduki mjini Mogadishu na watu wasiojulikana. Kila siku huwa
ninajiuliza, " Nani atafuatia?"
"Waandishi wa habari wa Somalia wanauliwa kwa sababu ya taaluma yao,"
alisema. Licha ya hayo, hatutaacha kazi yetu kwa kuwaogopa wanamgambo
kwa sababu tunahisi tunawatumikia watu kwa kuwapatia habari na ukweli
uliopo nyuma ya kile kinachotokea nchini."
Mohamed Abdullahi, mwandishi wa habari wa kujitegemea anayeishi
Mogadishu, alisema, "Mashambulizi dhidi ya waandishi wa habari wa
Somalia daima hayatasita. Kuna vyombo vingi nyuma ya hili, lakini
kikundi cha al-Shabaab chenye mafungamano na al-Qaida ndicho ni tishio
kubwa la kwa waandishi wa habari."
"Al-Shabaab wanawachukulia waandishi wa habari kama maadui wao
nambari moja kwa sababu [waandishi wa habari] wanaeneza ukweli na
kufichua uhalifu wa kikatili unaofanywa dhidi ya raia na kikundi hiki
kila siku," alisema.
No comments:
Post a Comment